EMAIL US AT info@wotesawa.or.tz
CALL US NOW +255-282-500-599
DONATE NOW

Shirika La WoteSawa Latoa Mafunzo Kwa Watoto Wafanyakazi Wa Nyumbani Jijini Mwanza.

Mkurugenzi wa Shirika la Wote Sawa la jijini Mwanza, Angel Benedicto, akiwaelekeza washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kisheria Watoto wafanyakazi wa nyumbani (CDWs), ili waweze kujisimamia wenyewe dhidi ya unyonyaji na unyanyaswaji unaofanya na baadhi ya waajiri.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Christina William akichangia mada katika mafunzo hayo

Washiriki wa mafunzo hayo wakimsikiliza Mkurugenzi wa Shirika la Wote Sawa la jijini Mwanza, Angel Benedicto

Washiriki wa mafunzo hayo ambao ni wafanyakazi wa ndani Watoto wakiendelea kusikiliza kile kinachoelekezwa na wawezeshaji wa semina hiyo.

Judith Ferdinand, Mwanza

Shirika la Kutetea Haki za Watoto Wafanyakazi wa Nyumbani (WoteSawa) la Jijini Mwanza limewapatia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kisheria jumla ya watoto 51, wanaofanya kazi za ndani, kutoka kata nne zilizopo wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Mafunzo hayo yaliofanyika kwa siku mbili tangu juzi katika hoteli Jijini Mwanza, yaliyoandaliwa na shirika hilo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutambua wajibu, haki na sheria zinazowalinda watoto hao ili waweze kijisimamia wenyewe dhidi ya unyonywaji na unyanyaswaji wanaoweza kukumbana nao.

Akizungumza na BMG, Mkurugenzi wa WoteSawa, Angel Benedicto, alisema wameandaa mafunzo hayo kwa wafanyakazi wa ndani kutokana na jamii kuwadharau hivyo kushindwa kujitetea na kuona aibu, kutojua wajibu,haki na sheria zinazowalinda.

Pia alisema kumekua na changamoto kwa baadhi ya waajiri kuwafanyisha kazi ngumu pamoja na biashara ya ngono jambo ambalo shirika hilo limeweza kufanya jitihada za kukabiliana nazo, kwa kufanya uchunguzi ambapo baadhi ya watuhumiwa wamekwisha fikishwa mahakamani.

Hata hivyo aliwaomba washiriki hao kuacha kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto wa waajiri wao kama kulipa kisasi na badala yake waripoti kwa ngazi husika,ili taratibu za kisheria zifuatwe.

Vilevile aliwaomba waajiri kuacha kuwafanyia vitendo vya ukatili wafanyakazi wa ndani kwa kuwapa adhabu kali ikiwemo kutowalipa mshahara, hali inayopelekea kufanya ukatili kwa watoto wao, na waachukulie kama sehemu ya familia.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo alisema baadhi ya waajiri wamekua wakikiuka masharti na kuwafanyisha kazi nzito ikiwemo kuwafurisha nguo zao za ndani, ambazo zinaweza kuwaletea madhara kiafya kama fangasi.

Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya waajiri kuwafanyisha biashara ya ngono na wakati mwingine vijana wao wa kiume kuwataka kimapenzi.

Deborah Miacheal ni mshiriki mwingine wa mafunzo hayo ambapo alisema kuwa amepata ujasiri wa kutetea haki na wajibu wake,endapo atafanyiwa vitendo vya kikatili na mwajiri wake ikiwemo kutolipwa mshahara.

Naye mshiriki Christina William alisema atatumia elimu hiyo kuwaelimisha wengine,ili kuweza kukomesha masuala ya unyanyasaji kwa wafanyakazi wa ndani,sambamba na kuwaomba waajiri kuwaruhusu wafanyakazi wao kuhudhuria mafunzo kama hayo.

Leave a reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *