Jeshi la polisi mkoani Mwanza limesisitiza kusimamia sheria ya mtoto ili kuhakikisha watoto chini ya umri wa miaka 14 hawatumikishwi katika shughuli mbalimbali ikiwemo kuajiriwa kufanya kazi za nyumbani.
Mrakibu Mwandamizi wa jeshi hilo mkoani Mwanza, Ally Mkalipa ameyasema hayo leo kwa niaba ya Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, kwenye kikao cha maafisa wa jeshi hilo mkoani Mwanza, kilichohudhuriwa pia na viongozi wa Shirika la Kutetea Haki za Watoto Wafanyakazi wa Nyumbani WoteSawa pamoja na Afisa Kazi mkoani Mwanza.
Katika kikao hicho, Shirika la WoteSawa limeshiriki ili kutoa chachu kwa maafisa wa polisi kama chombo kinachosimamia sheria kushiriki ipasavyo kuanzia ngazi ya nyumbani hadi kazini katika kulinda na kutetea haki za watoto wafanyakazi wa nyumbani na kuwanusuru na utumikishwaji.
Mkurugenzi wa shirika la WoteSawa, Angel Benedicto amesisitiza kuwa ni kosa kisheria mtoto chini ya miaka 14 kuajiriwa na kwamba mtoto chini ya miaka 18 lazima aajiriwe kufanya kazi zenye staha kwa ridhaa ya wazazi ama walezi hivyo jeshi la polisi liwe mstari wa mbele kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu.